Timu mpya kwenye mashindano ya klabu bingwa ya Afrika
Mashariki na Kati, Azam ya Tanzania, na vile vile mabingwa watetezi
Yanga, zimeingia fainali ya michuano hiyo ya Cecafa.
Azam imetinga fainali baada ya kuifunga Vita
Club ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo 2-1, wakati Yanga wamepenya
baada ya kuilaza APR ya Rwanda 1-0 kwenye mechi zilizochezwa Alhamisi
mjini Dar es Salaam.
Vita
walipata bao lao la kwanza kupitia kwa Alfred Mfongang na dakika tano
baadaye mchezaji mwenzake Isama Mpeko akatolewa nje baada ya kuonyeshwa
kadi ya pili ya njano.
Azam walitumia vyema upungufu huo kwa
kusawazisha kupitia kwa John Bocco dakika ya 68 na Mrisho Ngassa
akapachika bao la ushindi dakika ya mwisho wa mchezo.
Nao Yanga walipata bao lao dakika ya 13 ya kipindi cha nyongeza kupitia kwa mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda Hamis Kiiza.
Kiiza alifunga bao zuri la kichwa kufuatia mpira kutoka kwa Haruna Niyonzima, ambaye ni mchezaji wa kulipwa kutoka Rwanda.
Yanga na Azam watacheza fainali Jumamosi, mechi ambayo itatanguliwa na mechi ya kutafuta mshindi wa tatu kati ya Vita na APR. |
No comments:
Post a Comment