Klabu bingwa mtetezi Afrika Mashariki na Kati, Yanga
ya Tanzania, imefanikiwa kuingia nusu fainali ya mashindano ya Kombe la
Kagame baada ya kuitoa timu ya Mafunzo ya Zanzibar kwa mikwaju ya
penalti.
Matokeo hadi mwisho wa mchezo mjini Dar es
Salaam siku ya Jumatatu yalikuwa 1-1, Mafunzo wakiwa wa kwanza kupata
bao kipindi cha kwanza kupitia kwa Ali Mmanga.
Yanga
walifanikiwa kusawazisha dakika ya kwanza kipindi cha pili kupitia kwa
Said Bahanuzi na kufanya mchezo uamuliwe kwa penalti baada ya dakika
tisini, na Yanga kushinda kwa penalti tano kwa nne.
Yanga watacheza na APR ya Rwanda, ambao nao wametinga nusu fainali baada ya kuwatoa URA wa Uganda kwa mabao 2-1.
APR walipata mabao yao kipindi cha kwanza
kupitia kwa Jean Claude Iranzi na Seleman Ndikumana, wakati bao la URA
lilifungwa na Robert Ssentongo kipindi cha pili.
Kocha wa APR Mholanzi Ernest Bradnt anasema
itakuwa mechi ya kulipiza kisasi; “Yanga walitufunga hatua ya makundi,
hivyo tutahitaji kulipiza kisasi. Lakini pia tumeshinda kombe hili mara
tatu nyumbani na sasa tunataka kulishinda ugenini, hapa Tanzania,”
alisema.
Jumanne Simba itacheza na timu mpya kwenye
mashindano haya, Azam, pia kutoka Tanzania, na Vita Club ya Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Kongo itacheza na Atletico ya Burundi. |
No comments:
Post a Comment