Takribani mwezi mmoja baada ya kuandika
barua ya kugoma kuichezea timu ya taifa ya Cameroon, mchezaji
anayelipwa mshahara mkubwa zaidi duniani kwa upande wa soka duniani,
Samuel Etoo sasa anaonekana yupo tayari kwenda kinyume na msimamo wake
wa mwanzo na kurudi kuitumikia timu ya taifa lake baada ya kuwa na
mazungumzo na waziri mkuu wa nchi hiyo.
Mshambuliaji huyo
wa klabu ya Anzhi Makhachkala alifungiwa kwa miezi nane baada ya
kuongoza mgomo wa wachezaji dhidi ya Chama cha Soka cha Cameroon
kuhusiana na posho zao.
Hata alipomaliza kutumikia adhabu hiyo na
kuitwa kikosini, Eto'o alikataa na kusema kwamba hataichezea tena timu
ya taifa hadi hapo viongozi wa chama cha soka nchini mwake
watakapobadilika na kufanya kazi kwa weledi mkubwa na unaostahili.
Jambo hilo sasa
linaelekea kupata ufumbuzi baada ya Waziri Mkuu Philemon Yang kuzungumza
yeye mwenyewe na mtupia mabao huyo wa zamani wa Barcelona na kumuomba arudi
kikosini ili aisaidie nchi yake inayohaha kupata nafasi ya kufuzu kwa
fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2013).
“Mkuu
wa Nchi ameamua kulishughuilikia suala hilo yeye mwenyewe na ametupa
maelekezo,” amesema kocha wa Cameroon, Jean-Paul Akono.
“Baadaye
tulikutana kuweka mambo sawa na sasa kila kitu kiko vizuri. Hivi sasa
yuko tayari, lakini anaweza kukosekana kwa sababu ya majeraha.
Tutaendelea kuomba na kusubiri siku za mwisho kabla ya mechi."
Cameroon
walichapwa 2-0 katika mechi yao ya ugenini dhidi ya Cape Verde, ambayo
ni ya kwanza katika raundi ya mwisho ya kuwania kufuzu kwa fainali za
AFCON 2013, na kurejea kwa Eto’o kunatarajiwa kuwaongezea nguvu katika
mechi yao ya marudiano mjini Yaounde Oktoba 13. |
No comments:
Post a Comment