MWENYEKITI wa klabu ya Simba, Mhe;
Ismail Aden Rage, amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba wa
aliyekuwa msanii maarufu wa muziki na filamu, Hussein Ramadhani Mkiety,
maarufu kwa jina la Sharo Milionea, kilichotokea jana usiku mkoani Tanga.
Kwa niaba ya klabu ya Simba na kwa
niaba yake binafsi, Mwenyekiti anapenda kutuma salamu za pole kwa
familia ya marehemu, ndugu, jamaa na marafiki wote wa marehemu kutokana
na msiba huu mkubwa sana si kwao pekee bali kwa taifa zima la Tanzania.
Sharo Milionea hakuwa msanii wa kawaida.
Yeye ni miongoni mwa kizazi kipya cha
vijana wa Kitanzania walioamua kutafuta maisha kwa kutumia vipaji
walivyopewa na Mungu. Yeye alijitumbukiza zaidi katika uchekeshaji na
baadaye akaonyesha uwezo mkubwa katika fani ya muziki.
Sharo alikuwa maarufu kiasi kwamba
makampuni makubwa yalikuwa yameanza kumtumia kwenye matangazo yao ya
kibiashara. Hii ilionyesha kwamba makampuni yalibaini faida
itakayopatikana kwao kwa kumtumia msanii huyu ambaye bado alikuwa na
heshima kubwa kwenye jamii kutokana na haiba yake na uwezo wake kwenye
kazi alizokuwa akifanya.
Msiba huu umekuwa pigo kubwa kwa tasnia
ya filamu ambayo bado inaomboleza vifo vya wasanii kama Steven Kanumba,
Mlopelo na John Steven Maganga, waliofariki dunia mwaka huu pia.
"Ifahamike kwamba Sharo Milionea alikuwa miongoni mwa wasanii wa
Kitanzania waliotuma maombi Simba ya kutaka kushiriki kwenye mchakato wa
kutengeneza wimbo rasmi wa klabu ya Simba. Yeye alikuwa miongoni mwa
wasanii waliokuwa wakiumizwa na ukweli kwamba klabu kama Simba
inashindwa kufanya biashara ya kuuza nyimbo zake ilhali wanunuaji wapo,"
alisema Rage.
Kwa klabu ya Simba, namna pekee ya
kumuenzi marehemu ni kufanyia kazi mambo ambayo alikuwa akitushauri
kwenye eneo la biashara. Ni matumaini yetu kwamba iwapo tutafanya lile
alilokuwa akitushauri, atakuwa mwenye amani huko alikotangulia mbele ya
haki.
Rage amewaomba wasanii wa tasnia ya
filamu na muziki kuwa watulivu na wenye subra kwenye kipindi hiki kigumu
kwao. Kila kitu katika maisha ya wanadamu kinapangwa na Mwenyezi Mungu
na ndiyo maana Waswahili wana msemo kuwa Kazi ya Mungu haina makosa.
Mola na ailaze mahali pema peponi roho ya marehemu Hussein Ramadhani
Mkeity (Sharo Milionea). Imetolewa na Ezekiel Kamwaga Ofisa Habari Simba
SC. |
No comments:
Post a Comment