DORIS MALIYAGA NA CALVIN KIWIA
WACHEZAJI wapya waliosajiliwa na Simba wanatia raha. Kocha wa timu
hiyo, Milovan Cirkovic, amewaangalia akacheka halafu akatikisa kichwa
kuashiria kwamba kazi ipo.
Mastaa hao wapya waliosajiliwa wameonyesha uwezo, ubora na vipaji
vya aina yake ambavyo vimewakosha mashabiki wanaofurika Uwanja wa TCC
Sigara jijini Dar es Salaam kuzidi wale wanaoonekana katika mazoezi ya
watani wao, Yanga, wanaojifua Kijitonyama.
Wachezaji wapya waliosajiliwa na Simba ni pamoja na Abdallah Juma,
Paulo Ngalemwa, Kiggi Makassi, Waziri Hamad, Danny Mrwanda, Salim Kinje
na wale wa kigeni Wakongomani, Kanu Mbiyavanga na Lino Masombo na Mussa
Mudde wa Uganda.
Katika mazoezi yanayozidi kunoga, wachezaji hao wamekuwa wakionyesha
vitu vya aina yake licha ya kwamba mpaka sasa kiraka Mbiyavanga
ameonyesha kwamba ni balaa.
Ana kasi, nguvu, anajua kulazimisha na kwa nafasi kubwa amekuwa
akitumia akili ya ziada na mashabiki wametabiri kuwa akicheza na
Emmanuel Okwi basi Simba itakuwa moto.
Kwa kiwango chake kama hatampita beki, basi ni wazi anaweza kusababisha penalti muda wowote ule.
Kinje ni mzuri katika pasi za mwisho, pia kuchezesha timu kwa kasi ya aina yake na kupachika mabao kijanja.
Kiggi amewakosha mashabiki wa Simba kwa mashuti yake makali ya
kushitukiza na pia amekuwa akiwahadaa mabeki na kuwaweka kwenye wakati
mgumu.
Lino ndiyo usiseme. Mkongomani huyo aliyenyoa nywele staili ya
kiduku kama Mtaliano Mario Balotelli, amekidhi haja ya kocha wa Simba
ambaye alikuwa akitafuta beki wa kati mrefu kuliko Kelvin Yondani
aliyetimkia Yanga.
Lino, ambaye anazungumza lugha za Kilingala, Kifaransa na Kiswahili
kwa shida, ni mahiri kwenye kukaba, mipira ya juu na kuziba njia na
anatambia urefu wake kwani anamzidi Felix Sunzu.
Mudde ni kiraka kama Shomari Kapombe, kwani ameonyesha umahiri akicheza nafasi mbalimbali kwenye ulinzi na hata kiungo mkabaji.
Ufanisi huo wa wachezaji hao umelikosha benchi la ufundi na wameahidi makubwa kwa mashabiki kwa kuanzia na Kombe la Kagame.
Mudde aliyesajiliwa kutoka Sofapaka ya Kenya alisema: "Nimefurahi
kujiunga na Simba, mengi yamenivutia kuja kucheza hapa, kikubwa nataka
kufanya kazi kwanza ionekane uwanjani.
"Ninachowaahidi mashabiki sitawaangusha na wasubiri kazi yangu
uwanjani, kikubwa naomba ushirikiano kwao na wachezaji kwa ujumla."
Lino naye alisema: "Simba ni nzuri, nafurahi kujiunga nayo. Nafurahi
kuona mashabiki wakitupokea kwa furaha jambo ambalo sikulitegemea, nami
nawaahidi sitawaangusha."
Mashabiki ambao wanafika kwa wingi katika Uwanja wa Sigara, kama
kwenye mechi wamesikika wakisema kutakuwa na ushindani wa nguvu.
"Sijui nani ataanza, umemwona, Kinje, Abdallah na Kigi atacheza
mbele watatafutana ubaya pale maana wakiongezeka na wale wa zamani
patakuwa hapatoshi," mmoja wao alisikika akisema.
Milovan amesifu wachezaji hao akisema: "Wachezaji wapya nimewaona,
wote ni wazuri. Kutakuwa na mabadiliko kikosini na tutakuwa na timu bora
zaidi ya msimu uliopita. Nina raha sana."
Simba, ambayo ndiyo timu iliyotwaa mara nyingi zaidi Kombe la Kagame
imepangwa Kundi A ikiwa na timu za Vita Club ya DRC, URA ya Uganda na
Ports ya Djibouti. Simba itafungua dimba na URA, Julai 16 wakati
michuano itaanza Julai 14. |
No comments:
Post a Comment