Chama cha soka cha England, FA, kimetozwa faini ya
Euro 5,000 (sawa na pauni 4000), kutokana na utovu wa nidhamu wa
mashabiki wake ambao Ijumaa iliyopita walijaribu kuuvamia uwanja baada
ya Engldan kuishinda Sweden.
Faini hiyo ni kufuatia mashabiki kujaribu
kuingia uwanjani baada ya England kuishinda Sweden 3-2 katika mechi ya
kundi D mjini Kiev.
Chama
cha FA kimeamua hakitakata rufaa kuhusiana na faini hiyo, na kwa kuwa
UEFA haijaitoza FA pesa nyingi, inaashiria kwamba shirikisho hilo la
soka ya Ulaya linalichukua tukio hilo kama jambo dogo.
"Tunakubali hatua iliyochukuliwa, na tunalifikiria tukio hili kama jambo ambalo limetatuliwa," taarifa ya FA ilielezea.
Baada ya magoli ya England yaliyotiwa wavuni na
Theo Walcott na Danny Welbeck, mashabiki kati ya 20 hadi 30
walivikaribia vizuizi uwanjani, na kutaka kuingia ndani ya uwanja wa
Olympic, lakini walifanikiwa kuifikia sehemu ya riadha tu.
Chama cha FA, kikijitetea, kiliweza kutoa
ushahidi thabiti wa video mbele ya UEFA na kuonyesha kwamba “uvamizi”
huo ulikuwa ni jambo ambalo lilitokea ghafula, na wala mashabiki hao
hawakuwa wamepanga kutekeleza kitendo hicho.
Tukio hilo lilichukuliwa kama jambo dogo, na
hata afisa wa UEFA katika mechi hiyo hakulitaja katika ripoti yake
kuhusiana na mechi.
Chama cha FA pia kimethibitisha kwamba hakuna
mashabiki wa England waliokamatwa aidha nchini Poland au Ukraine katika
mashindano ya mwaka huu.
|
No comments:
Post a Comment