PSI

PSI

Monday, August 20, 2012

Mchina awa Miss World, Tanzania kama kawa

KWA mara nyingine Tanzania imeendelea kuwa mshiriki na siyo mshindani katika shindano ya Miss World baada ya kuambulia patupu huku mshiriki kutoka China, Yu Wenxia, akiibuka kidedea kwa kutwaa taji hilo, juzi  jijini Ordos, China.
Hii inakuwa mara ya pili kwa mrembo kutoka China kutwaa taji hilo ndani ya kipindi cha muda mfupi, kwani mwaka 2007, taji hilo lilienda kwa Zhang Zilin.
Katika shindano hilo ambalo Tanzania iliwakilishwa na Lisa Jensen (picha ndogo), mshindi wa pili alikuwa Sophie Elizabeth Moulds wa Wales huku Jessica Michelle Kahawaty wa Australia akishika nafasi ya tatu.
Yu mwenye umri wa miaka 23 ni mwanafunzi anayejifunza masuala ya muziki.
“Nilipokuwa mdogo nilijihisi nina bahati sana kwa kuwa watu wengi walinisaidia, nadhani siku zijazo nami nitawasaida watoto wengi wawe na bahati,” alisema Yu.
Taji la mwaka uliopita lilikuwa likishikiliwa na Ivian Sarcos wa Venezuela.
Mara ya mwisho kwa Tanzania kufanya vizuri ilikuwa ni kupitia kwa Nancy Sumari ambaye alikuwa Miss World Africa, yaani alishika nafasi ya juu katika warembo wote kutoka Bara la Afrika mwaka 2005.

No comments: