UONGOZI wa Simba umesema unaandaa sherehe maalum ya kumuaga aliyekuwa
mchezaji wake, Ulimboka Mwakingwe, baada ya kuichezea timu hiyo kwa muda
wa miaka 10 hadi kufikia hatua ya kustaafu soka. Akizungumza na
Championi Jumatatu, Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga, alisema
klabu hiyo itaandaa mechi maalum ambayo Ulimboka atacheza huku akiwa
amevaa jezi yake namba 14, ikiwa ni ishara ya kumuenzi pamoja na
kumtunukia heshima maalum ya kuichezea timu hiyo kwa muda wote huo. “Mchezaji
wetu Ulimboka Mwakingwe amestaafu soka rasmi, hivyo uongozi utaandaa
sherehe maalum ya kumuaga, ikiwa ni pamoja na kumtunukia heshima maalum
kutokana na kuichezea Simba kwa muda mrefu. “Katika sherehe hizo,
mchezaji huyo atacheza mechi moja ya kuagwa na timu tutakayoitafuta hapo
baadaye na atavaa jezi yake namba 14 ikiwa ni ishara ya kumpa heshima,”
alisema Kamwaga. Alisema kuwa kufanya hivyo kutamsaidia mchezaji
huyo kufarijika kutokana na mchango wake mkubwa alioutoa kwa Simba
katika muda wote alioitumikia klabu hiyo. Ulimboka alishindwa
kumalizia ligi msimu uliopita kutokana na kukabiliwa na kesi ya kutoa
rushwa kwa kipa wa Mtibwa Sugar, Shaban Kado, ili aachie mabao katika
mechi ya Simba dhidi ya timu hiyo msimu wa 2010/11. Wakati huo yeye
alikuwa Majimaji. |
No comments:
Post a Comment