Kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania
(Taifa Stars) kikiwa na wachezaji 17 kimewasili leo asubuhi jijini
Gaborone tayari kwa mechi ya kirafiki ya kalenda ya Shirikisho la
Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) dhidi ya wenyeji Botswana 'Zebras'
itakayochezwa kesho (Agosti 15 mwaka huu).
Stars ilitua kwenye
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sir Seretse Khama saa 5.45 asubuhi kwa
saa za hapa ambapo nyumbani ni 6.45 na kupokewa na viongozi wa Chama cha
Mpira wa Miguu Botswana (BFA) na Watanzania wanaoishi hapa Botswana.
Baadhi
ya wachezaji walioko kwenye kikosi hicho ni Frank Domayo, Ramadhan
Singano na Simon Msuva ambao walijiunga na Stars saa chache baada ya
kurejea kutoka Nigeria ambapo walikuwa na timu ya vijana wenye umri
chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes) ambayo Jumapili ilicheza mechi ya
mashindano ya Afrika dhidi ya Nigeria (Flying Eagles).
Wachezaji
wengine kwenye kikosi kilichoko Botswana ni Aggrey Morris, Amir Maftah,
Athuman Idd, Erasto Nyoni, Haruna Moshi, Juma Kaseja, Kelvin Yondani,
Mrisho Ngassa, Mwadini Ally, Mwinyi Kazimoto, Ramadhan Chombo, Salum
Abubakar, Said Bahanuzi na Shabani Nditi.
Stars inayodhaminiwa
na Kilimanjaro Premium Lager imefikia kwenye hoteli ya Oasis ambayo pia
ndipo Zebras imepiga kambi kwa ajili ya mechi hiyo. Mechi itaanza kesho
saa 1 kamili usiku kwa saa za hapa na itafanyika kwenye Uwanja wa
Molepolole Sports Complex. Uwanja wa Taifa wa Botswana hivi sasa uko
kwenye matengenezo.
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen amesema mechi hiyo ni muhimu kwa vile timu yake bado inakabiliwa
na mechi za Kombe la Dunia Kanda ya Afrika, na michuano ya Kombe la
Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) inayotarajia kuanza baadaye mwaka
huu. |
No comments:
Post a Comment