Kocha mkuu mpya wa Yanga, Tom
Saintfiet, ambaye jana jioni alitarajiwa kusaini mkataba wa kukinoa
kikosi cha timu hiyo, amezuia mechi za kirafiki mpaka baada ya
kumalizika kwa Kombe la Kagame la klabu bingwa za Afrika Mashariki na
Kati.
Kocha huyo aliyewasili nchini juzi, alisema hataki timu hiyo icheze
michezo ya kirafiki kwa kuwa ana muda mchache wa kuiandaa kwa ajili ya
Kombe la Kagame na pia hataki kuchosha wachezaji wake.
Akizungumza kwenye mazoezi ya timu hiyo kwenye Uwanja wa Kaunda, raia wa
Ubelgiji Saintfiet, alisema anataka kuwaangalia zaidi wachezaji wake
kwenye mazoezi ya timu hiyo.
Pia, alisema atakazania zaidi mazoezi ili kupata kikosi kitakachokuwa na
uwezo wa kutetea ubingwa wa mashindano hayo ya kila mwaka.
"Kama ni michezo ya kirafiki ni vizuri ikiwa tutacheza baada ya Kagame
(kwasababu) kwa sasa nina muda mchache wa kuandaa timu," alisema.
"Wachezaji bado sjawajua na naamini mazoezini ndipo nitakapopata nafasi ya kuwaona na kujua uwezo wa kila mchezaji."
Kwa muda mfupi aliohudhuria mazoezi ya timu hiyo, kocha huyo alisema, amegundua Yanga ina wachezaji wenye vipaji vya soka.
"Nafikiri haitaniwia vigumu kwangu kufundisha... wachezaji niliowakuta
wanaonekana wana uwezo mkubwa wa kucheza soka," alisema Saintfiet ambaye
ametoka tu kuwa kocha wa timu ya taifa ya Ethiopia lakini pia amewahi
kuwa mwalimu wa Zimabwe na Namibia.
Kwa upande wake, Afisa Habari wa klabu hiyo, Luis Sendeu alisema uongozi
umekubaliana na maamuzi ya kocha huyo na kusisitiza kuwa mchezo wao wa
kirafiki dhidi ya Bunamwaya ya Uganda uliokuwa uchezwe kesho, umefutwa.
Sendeu alisema kutokana na ushauri wa kocha, kikosi hicho kitaendelea na mazoezi kwa ajili ya kujiandaa na mashindano ya Kagame.
Yanga imepangwa kufungua dimba dhidi ya Atletico ya Burundi Julai 14 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
|
No comments:
Post a Comment