Klabu mbalimbali
zimewasilisha pingamizi Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
kupinga usajili wa wachezaji 17 walioombewa usajili katika timu za Ligi
Kuu.
Toto Africans imewawekea
pingamizi wachezaji Enyinna Darlinton aliyeombewa usajili Kagera Sugar,
na Mohamed Soud anayekwenda Coastal Union kwa maelezo kuwa bado ina
mikataba na wachezaji hao.
Pia Flamingo ya Arusha
inapinga usajili wa wachezaji wake Kelvin Friday Iddy katika timu za
Azam na Salim Walii (Polisi Mara) kwa vile taratibu za kuwahamisha bado
hazijafanywa. Nayo Kagera Sugar inapinga usajili wa beki David Charles
Luhende kwenda Yanga kwa vile ada ya uhamisho haijalipwa.
Super Falcon ya
Chanjamjawiri, Chakechake, Pemba inapinga wachezaji wake wanne; Edward
Christopher Shija, Samir Said Luhava (Simba), Robert Joseph Mkhotya
(African Lyon) na Sultan Juma Shija (Coastal Union) kusajiliwa katika
timu hizo kwa maelezo taratibu halali za uhamisho hazikufuatwa.
Mchezaji Othman Hassan
aliyeombewa usajili Coastal Union anapingwa na Oljoro JKT kwa vile bado
ana mkataba na timu hiyo unaomalizika Mei 24, 2013. Nayo Rollingstone
Multipurpose Ateclass Foundation ya Arusha inapinga usajili wa Kigi
Makassy kutoka Yanga kwenda Simba hadi itakapolipwa fidia ya kumlea
mchezaji huyo kwa vile bado hajafikisha umri wa miaka 23.
Azam inapinga usajili wa
Ramadhan Chombo ‘Redondo’ kwenda Simba kwa maelezo bado ina mkataba naye
unaomalizika Juni 11 mwakani. Nayo Simba inapinga Kelvin Yondani
kusajiliwa Yanga kwa maelezo kuwa ina mkataba naye uliosainiwa Desemba
23 mwaka jana.
Vilevile Simba imewasilisha
malalamiko ya mchezo usio wa kiungwana katika usajili wa Mbuyu Twite
aliyeko Yanga kwa maelezo alisaini mkataba na klabu yao Agosti Mosi
mwaka huu mbele yao, viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Rwanda
(FERWAFA) na APR ambapo alilipwa dola 30,000 na nyingine 2,000 ikiwa ni
fedha ya kujikimu na nauli yake ya kujiunga na klabu hiyo.
Nayo Yanga inapinga Simba
kuwaacha wachezaji Dan Mrwanda, Haruna Shamte, Kanu Mbiyavanga na Lino
Masombo kwa maelezo walishapatiwa leseni za kucheza Ligi ya Tanzania
walizozitumia kwenye mashindano ya Kombe la Kagame. Pia inapinga
Ramadhan Chombo ‘Redondo’ kujiunga Simba kwa vile ana leseni ya kuchezea
Azam kwa msimu wa 2012/2013.
Pingamizi lingine la Yanga
kwa Simba ni kuwa imezidisha idadi ya wachezaji wa kigeni wanaotakiwa
kusajiliwa kwa maelezo inao wanane wakati wanaoruhusiwa ni watano.
Imewataja wachezaji hao kuwa ni Lino Masombo, Felix Sunzu, Emmanuel
Okwi, Mussa Mude, Kanu Mbiyavanga, Pascal Ochieng, Komalmbil Keita na
Daniel Akuffor.
Kamati ya Sheria, Maadili na
Hadhi za Wachezaji ya TFF chini ya Mwenyekiti wake Alex Mgongolwa
inatarajia kukutana Jumapili (Septemba 2 mwaka huu) kupitia pingamizi
hizo pamoja na usajili wa wachezaji kwa ujumla kwa 2012/2013.
Redondo, Luhende, Christopher Edward, Kiggy Makasi na Yondani wawekewa pingamizi kucheza ligi kuu.
|
No comments:
Post a Comment